Friday, October 31, 2008

“VIJANA TUFIKIRI NA KUUNGANA KUKOMBOA AFRIKA”



TAARIFA KWA UMMA

SALAMU ZA MSHIKAMANO KATIKA SIKU YA VIJANA AFRIKA

“VIJANA TUFIKIRI NA KUUNGANA KUKOMBOA AFRIKA”

Novemba Mosi ni siku ya Vijana Afrika. Siku hii imepitishwa na Umoja wa Afrika kama siku maalum ya kuadhimisha na kutafakari mchango wa vijana katika maendeleo ya bara letu kiuchumi, kisiasa na katika nyanja mbalimbali za jamii. Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA), napenda kuungana na vijana wote barani Afrika katika kuadhimisha siku hii.

Kama sehemu ya maadhimisho hayo, vijana wa CHADEMA wamepanga kufanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama Novemba Mosi ili kuzungumzia hali ya siasa, uchumi na kijamii katika bara la Afrika katika muktadha wa changamoto zinazowakabili vijana na fursa ambazo zinaweza kutumika.

Nachukua fursa hii kutoa salamu za mshikamano kwa vijana wote kuungana kuitumia siku hii kutafakari nafasi na wajibu wa vijana katika kuleta demokrasia na maendeleo katika bara la Afrika.

“Vijana wa zamani kama Mwalimu Nyerere, Nkurumah Mandela na wengineo walitumia ujana wao kupambana na ukoloni, na kuleta uhuru katika mataifa yao. Ni wajibu wa vijana wa sasa kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na ushindani wa kibeberu unaoliathiri bara la Afrika nyuma ya kivuli cha utandawazi. Vijana wanaweza kutekeleza wajibu huu vizuri kama watathubutu kufikiri na kufikiri kuthubutu kuunganisha nguvu bila kujali mipaka ya nchi, hali au itikadi”

Bara la Afrika ni bara ambalo limejaliwa rasilimali, lakini rasilimali hizi zimegeuzwa na watawala kuwa laana(resource curse) yenye kuchochea vita na kuongezeka masikini kwa wananchi walio wengi hususani vijana.

Tunachukua fursa hii kuwataka vijana wa Afrika badala ya kuelekeza nguvu zao kutumika katika vita na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe watumie nguvu hizo kupambana na ufisadi, kutetea rasilimali na kuleta mabadiliko katika mataifa yao kupitia fikra mbadala.

Nafasi ya vijana kuleta ukombozi katika bara ni kubwa kama vijana watatumbua kwamba bara la Afrika lina uwingi mkubwa wa vijana kuliko makundi rika mengine; na kwamba vijana wakijitazama na kutazamwa kama suluhisho badala ya tatizo wanaweza kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya bara letu.

Ni vyema, waunda sera na watoa maamuzi barani Afrika wakatambua uwepo wa ongezeko kubwa la idadi ya vijana(youth population bulge) na kwamba wachukulie hali hii kuwa ni fursa badala ya tatizo. Bila hali hii kutambuliwa rasmi na kuundiwa sera na mikakati, matatizo yanayowakabili vijana mathalani ongezeko la ukosefu wa ajira, upungufu wa fursa za kielimu, mmomonyoko wa maadili, ongezeko la matumizi ya madawa ya kulevya na kusambaa kwa ugonjwa wa VVU/UKIMWI miongoni mwa vijana yatazidi kushamiri.

Changamoto ya ongezeko la vijana Afrika inaathiri zaidi miji mikubwa katika Afrika kutokana na kasi ya vijana kutoka vijijini kukimbilia mijini kutafuta fursa za maisha. Hivyo, katika kuadhimisha siku ya vijana Afrika kwa mwaka huu, mkazo uwekwe katika kuhamasisha uwepo wa mazingira ya kuboresha sekta zinazogusa vijana wengi Afrika hususani kwa kuboresha kilimo. Pia, sekta za rasilimali Afrika mathalani uchimbaji madini na mafuta ziwekewe mazingira ya kutoa ajira kwa vijana walio wengi badala za sekta hizo kutawaliwa na makampuni makubwa ya kigeni. Hata pale sekta hizo zinapotawaliwa na uchimbaji mkubwa mkazo uwekwe kuhakikisha muunganiko wa mbele na nyuma(forward and backward linkage) na sekta nyingine za kiuchumi.

Ili kuhakisha kwamba nguvu ya umma ndio inakuwa msingi wa uongozi katika Afrika, vijana wachukue hatua za kulinda demokrasia Afrika ambayo imeanza kutetereshwa na utadamuni ambao unaoendelea katika bara hili wa kung’ang’ania madaraka. Utamaduni huu unachukua sura ya baadhi ya nchi kutawaliwa kijeshi lakini pia unachukua sura ya ung’ang’anizi wa madaraka hata baada ya chaguzi kutaka vingenevyo kwa kutumia mwanya wa uundaji wa serikali za mseto ama za umoja wa kitaifa kama njia ya kuepusha migogoro.

Mwisho, ili kuwa na muongozo wa pamoja katika kuwezesha vijana kutimiza wajibu wao katika bara la Afrika, tunatoa rai kwa serikali za Afrika ambazo hazijaridhia bado Mkataba ya Vijana wa Afrika(African Youth Charter) ulipitishwa na viongozi wa umoja wa Afrika mwaka 2006 mjini Banjul nchini Gambia kufanya hivyo mara moja. “Na katika hili, namtaka Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aonyesha mfano mzuri kwa wenzake kama kweli wamedhamiria kuweka mstari wa mbele kushughulikia masuala ya vijana. Inashangaza kwamba mpaka pamoja na Rais Kikwete kusaini mkataba huo mwaka 2006 akiwa mjini Banjul, mpaka sasa mkataba huo haujaridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila mwaka, kuanzia wakati huo mpaka sasa, Wizara inayohusika na masuala ya vijana imekuwa ikitoa kauli kwamba mkataba huo utaridhiwa ‘kikao kijacho cha bunge’. Hata hivyo vikao vingi vimepita bila mkataba huo kuridhiwa; wakati sasa umefika wa Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri kuiwajibisha hadharani wizara inayohusika kwa kuchelewa kutimiza wajibu huu muhimu wa maendeleo ya vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla”

Ujumbe huu umetolewa Mwanza-Tanzania 31 Oktoba 2008 na:

John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa