Tuesday, October 20, 2009

Maandamano

Oktoba 14, niliongoza maandamano ya kumbukumbu ya Nyerere. Wapo waliunga mkono, wapo waliokosoa. Kwa wakosoaji, hoja mbili kubwa ziliibuliwa; mosi, kwa viongozi wa CHADEMA kumuenzi Mwalimu, na kwamba kumuenzi huko ni utamaduni ule ule wa kusifu na kuabudu viongozi. Ulikuwepo pia mtazamo kwamba kumuenzi kwa maandamano badala ya kufanya shughuli nyingine ni kupoteza muda. Katika kundi hilo, wapo waliopendekeza kwamba tulipaswa kumuenzi kwa njia nyingine mathalani kusafisha mazingira nk!.
Tuliamua kufanya 'maandamano'(sio matembezi) kufikisha ujumbe mahususi wa mabadiliko. Kati ya mambo ambayo tulikuwa na ubishani na polisi ni kuomba kibali cha maandamano badala ya matembezi. Nashukuru kwamba polisi walitupa kibali, hata hivyo, nilieleza masikitiko yangu kuwa baada ya kutoa kibali na taarifa kuanza kusambaa; polisi hao hao wakaaandika barua nyingine ya kufuta kibali. Maelezo ya kikao nao ni kwamba maandamano yangepunguza 'attention' kwa hotuba ya rais Butiama, na pia ya kwamba siku ya Nyerere ni ya maombolezo ya kifo; hivyo si vyema kufanya maandamano. Tulikuwa na mjadala wa zaidi ya masaa kadhaa mpaka usiku. Nampongeza kamanda wa polisi mkoa, kwa kuwa hatimaye baadaye aliacha kutupatia barua ya kufuta maandamano. Nashukuru kwamba alitambua kwamba uamuzi wa kufuta maandamano yale ulikuwa kinyume cha katiba, na hakukuwa na sheria yoyote ambayo ilimpa mamlaka hayo(sheria inazungumza sababu za kiusalama).
Tulifanya maandamano kwa lengo la kufikisha ujumbe, kwamba Nyerere anaenziwa kinafiki na watawala, na chama chao. Njia za kupitia maandamano hayo tulizipanga kwa sababu maalumu; maandamano hayo yalianzia Uwanja wa Tanganyika packers; pembeni ya magofu ya kiwanda ambao kilibeba maadhui ya sera za mwalimu za kuweka kipaumbele uzalishaji wa ndani. Magofu ya kiwanda kile, ni ishara ya sera mbovu za CCM ya sasa, za kutanguliza ubinafsi kwa kisingizio cha ubinafsishaji kuuza viwanda kwa bei chee. Na kugeuza nchi kuwa soko holela!.Tulipotoka hapo, tulipita Msasani/Mikocheni kwa Mwalimu, pale tulisimama kwa dakika moja kumkumbuka; pembeni yetu kikiwepo kiwanja cha wazi ambacho bila nguvu ya umma, tayari kilishatekwa kinyemela karibu kabisa na macho ya Nyerere!Tukaelekea mpaka Kinondoni; tukipita katika maeneo yanayowakilisha kuongezeka kwa pengo baina ya matajiri na masikini katika nchi yetu. Tukapita makao makuu ya chama, ilikuwa Dr Slaa atusalimu, lakini baada ya kuwa ameshasikia hotuba ya Kikwete na namna ambavyo aligeuza maadhimisho ya Nyerere ya kitaifa kuwa ya CCM, Dr Slaa akaamua kujiunga nasi kuendelea na maandamano ili kutoa ujumbe maalum.Tukafika ofisi ya Mkoa wa kichama wa Kinondoni ya CHADEMA, pale Dr Slaa akahutubia(Mwenye audio ya Hotuba yake atuwekee maana alisema maneno mazito sana kuhusu polisi, Kikwete na mwelekeo wa taifa)
Kwa sababu mbalimbali, tulikatishia maandamano hapo; lakini itakumbukwa kwamba kwa mujibu wa ratiba niliyoisambaza awali; maandamano yalikuwa yaendelee kupitia Magomeni, Mburahati, Makurumla, Manzese mpaka Ubungo.Pale Magomeni, ilikuwa tusimame kwenye nyumba ya kwanza kabisa aliyoishi Mwalimu ambayo alipangishiwa na wazee wa Dar es es salaam wakati wa harakati za kudai uhuru. Ilikuwa tuwe na ujumbe maalumu pale, kuhusu mchango wa wazee wa Magomeni, Kinondoni na DSM kwa ujumla katika harakati za kudai uhuru. Na wajibu wao wakati huu katika kuleta mabadiliko baada ya misingi ya taifa hili kutikiswa na maadili kutekelezwa. Hata nyumba hii ambayo imebeba kumbukumbu ya historia kwa bahati mbaya nayo imeshavunjwa.
Pale Urafiki, ilikuwa tusimame tena katika kukumbuka mchango wa Mwalimu; katika kujenga viwanda vyenye muunganiko wa mbele na nyuma(foward and backward) na sekta zetu za kiuchumi. Kiwanda cha nguo cha urafiki, sasa uzalishaji umepungua, mitambo mingine imeuzwa kama vyuma chakavu, nyumba za wafanyakazi zimeuzwa kinyemela; wafanyakazi wanateseka kwa maslahi duni; maghorofa yale yanakodishwa kwa watu tofauti kibiashara badala ya makusudio ya awali. Ilikuwa tusimame kituo cha mabasi Ubungo, pale ilikuwa tuweke bayana ufisadi wa pale na ukikukwaji wa sheria katika zabuni. CAG tayari alishakamilisha ripoti ya ukaguzi mpaka leo Waziri Mkuu Pinda ameikalia. Lakini nilidokeza nikiwa pale Kinondoni, UBT ni mfano wa namna ambavyo makada wa CCM wanaojigamba kumuenzi Mwalimu walivyomsaliti; mradi ule uko chini ya familia ya Kingunge Ngombare Mwiru; mwenye kujiita mjamaa, kumbe ni kiwakilishi cha tamaa za viongozi hao. Matokeo ya Maamuzi ya Zanzibar yaliyofukia miiko ya uongozi.
Ilikuwa tutoke pale, tusonge mbele tukipita makao makuu ya msururu wa Majenereta ya umeme kuanzia Songas, Dowans nk; jirani kabisa na Makao Makuu ya TANESCO. Kiwakilishi cha CCM ya leo, wakati wa mwalimu aliona mbali na kuwekeza katika miradi ya muda mrefu ya nishati; CCM ya leo, inaendesha nchi kwa dharura; lakini pia njia ile ni ishara ya namna wananchi wanavyonywa katika sekta ya nishati ya umeme kupitia mikataba ya kifisadi kwa barakoa ya capacity charges nk. Pale ilkuwa turudie tena mwito wetu wa miaka kadhaa nyuma, wa kutaka mitambo ile ya Dowans itaifishwe; wakati huo huo taifa lichague uongozi na sera mbadala zitakazosimamia uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya nishati wa taifa letu.
Naandika ujumbe huu leo; kwa sababu bado naamani, maandamano yale yanapaswa kuendelea; kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere haipaswi kuwa ya siku moja, ni suala endelevu kwa vitendo. Naandika ujumbe huu kuuliza kama kuna ambao wako tayari kuunga mkono maandamano haya ya safari ya pili kufikisha ujumbe huu.
Naandika ujumbe huu mgao wa umeme ukiwa unaendelea; naandika ujumbe huu ikiwa Zitto na viongozi wengine wamerudia tena mwito wa kutaka mitambo ile itaifishwe. Naandika ujumbe huu nikijua kwamba tunahitaji masuluhisho ya muda mfupi ya dharura, lakini pia tunahitaji kufikiria masuluhisho ya muda mrefu. Kuna ambaye yupo tayari kuandamana? Iwe kwa yeye mwenyewe au kuwezesha watanzania wengine kuandamana? Tafadhali tuwasiliane kupitia 0784222222 au mnyika@yahoo.com.
Tunaweza tukatoa matamko kwenye vyombo vya habari, tunaweza tukajenga hoja bungeni, tunaweza tujadili kwenye makongamano. lakini tukumbuke pia, tunawajibu wa kuunganisha nguvu ya umma. Maandamano ni njia mojawapo ya kufikia azma hiyo. Iwe ni maandamano ya kulaani ama kutoa ujumbe mbadala. Iwe ni kuonyesha hasira ya kutopata tunachostahili kupata ama ni kushinikiza kupata tunachopaswa kupata. Tukubali kuwa mawakala wa mabadiliko tunayotarajia kuyaona. Pamoja tunaweza!

No comments: