Thursday, December 23, 2010

Serikali itoe tamko vurugu Arusha

KATIBU wa Kambi ya Upinzani Bungeni,John Mnyika amelitaka Jeshi la Polisi, Waziri Mkuu, Ofisi ya Bunge na chama tawala cha CCM kutoa tamko kuhusu kitendo cha kupigwa kwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Lema alipigwa vibaya na askari wa Jeshi la Polisi wakati alipokwenda kwenye mkutano wa madiwani kupinga uchaguzi wa meya wa Jiji la Arusha, akidai kuwa mkutano huo wa uchaguzi uliitishwa kinyemela kwa kushirikisha madiwani wa CCM na TLP tu.

Katika mkutano huo wa uchaguzi, diwani wa CCM wa Kata ya Olorien, Gaudence Lyimo alichaguliwa kuwa meya na nafasi ya naibu meya kwenda kwa diwani wa Kata ya Sokoni (TLP), Michael Kivuyo.
Mnyika, ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema ameshangazwa na tukio hilo kwa kuwa polisi wameamua kuwapiga wananchi ambao hawakufanya fujo wala kuwa na silaha ya aina yoyote.

“Tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema kutoa tamko kali dhidi ya askari polisi waliohusika kupiga wananchi, akiwemo mbunge wa Chadema,” alisema Mnyika.

“Picha zipo wazi na askari waliohusika katika tukio hili na wanaonekana wazi, kwa hiyo IGP pia achukue hatua kali kwa askari waliohusika. Hakuna sheria inayomtaka polisi kupiga raia ambao hawakufanya fujo wala kuwa na silaha za aina yoyote.”
Alisema pia anamtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa tamko la kulaani kitendo hicho kwa kuwa limetokea katika uchaguzi wa Umeya ambao kimsingi upo chini ya Wizara ya Tamisemi.

“Ili uingie bungeni kama si mbunge kuna kanuni na taratibu zake, sasa iweje leo polisi waingie katika mkutano wa baraza la madiwani tena wakiwa na silaha,” alihoji Mnyika.

Mnyika alifika mbali na kusema kuwa pia Ofisi za Bunge zinatakiwa kulitolea tamko tukio hilo kwa kuwa linamhusu mbunge ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake na kwamba kitendo cha kupigwa ni sawa na kuingilia maslahi ya mbunge.
“Chadema nao wanatakiwa kulitolea tamko tukio hili, nasema hivi kwa kuwa Chadema iliwahi kusema kuwa vyombo vya dola ndio vitakavyosababisha umwagaji damu na jambo hilo limedhihirika wazi,” alisema Mnyika.
“Hata CCM nao wanatakiwa kusema kitu kuhusiana na suala hili kwa kuwa ulikuwa uchaguzi unaokihusisha chama hicho.”
Lakini imesema itakuwa vigumu kutoa tamko au kulizungumzia suala hilo kwa kuwa lina mwelekeo wa kisheria.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili na kueleza kuwa hata hivyo serikali haina taarifa ya kupigwa kwa mbunge huyo.

“Siwezi kuzungumza lolote kuhusu tukio la kupigwa kwa Mbunge Lema, kwa kuwa bado sijapata taarifa rasmi ya tukio hilo. Nimelisikia kupitia vyombo vya habari,’’ alisema Lukuvi.
Wakati huohuo, hali ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema inaendelea vizuri na sasa ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Mbunge huyo aliliambia gazeti hili jana kuwa aliruhusiwa kutoka hospitalini juzi saa 1:30 usiku baada ya kuona hali yake inaendelea vizuri.

Lema alisema baada ya kufanyiwa vipimo mbalimbali madaktari hao walibaini kuwa alipatwa mshituko wa shinikizo la damu kutokana na kipigo hicho cha polisi.
“Ni ajabu sana polisi kupiga raia kama mimi hovyo; nimeumia sana na nimedhalilishwa lakini ninajiandaa kuwachukulia hatua kwa kuwa nawajua kwa sura na nitaendelea kupambana kudai haki yangu hadi kieleweke,” alisema mbunge huyo
Diwani wa Kata ya Elerai (Chadema), John Bayo alisema leo wanatarajia kwenda mahakamani kufungua kesi kupinga uchaguzi huo kutokana na baadhi ya kanuni kutofuatwa.

Chanzo: Mwananchi (20 Disemba 2010)

No comments: