Monday, January 10, 2011

Hoja ya Katiba Mpya bado ipo

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amesema taarifa ya hoja ya mabadiliko ya Katiba aliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge iko pale pale na mchakato wa kupata maoni ya wananchi na wataalamu wa sheria utaendelea kama ilivyokusudiwa awali.

Mnyika alieleza hayo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kusisitiza muhimu wa hoja hiyo kurejeshwa kwa wananchi kupitia chombo cha uwakilishi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema hatua hiyo inatokana na kupokea ushauri na kutakiwa kuendelea na hoja ya mabadiliko ya Katiba mpya baada ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu Katiba mpya kuacha kutoa ufafanuzi kuhusu mchakato wake.

Mbunge huyo alisema Rais Kikwete alionyesha bayana hana mpango wa kuhusisha umma kuanzia hatua za awali, hivyo kupitia kuwasilisha hoja au muswada bungeni ili kuwekwa mfumo wa kisheria wa kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa kuandikwa kwa Katiba mpya ya Tanzania.

“Kuna ushahidi kuwa serikali ya Rais Kikwete haina dhamira ya kuandika Katiba mpya inayohusisha umma na badala yake kuendeleza hodhi ya serikali ambayo inaweza kusababisha mapitio yenye kasoro za miaka yote,“ alisema mbunge huyo.

Alisema hatua hiyo ya Rais Kikwete, inadhihirisha anaitaja Katiba mpya kwa maneno bila kuonyesha vitendo kuwezesha mchakato huo kwa kuushirikisha umma kwa ukamilifu.

“Kutokana na maoni niliyopokea na utata wa kauli za serikali kuhusu mchakato wa Katiba mpya naendelea kukamilisha taratibu za kuwasilisha hoja binafsi kwenye Bunge la Februari kuhusu mchakato wa Katiba mpya,” alisema Mnyika.

Alisema kutokana na mjadala unaoendelea inaonekana ipo haja ya suala hilo la mchakato wa Katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea Ibara ya 8 ambayo inatamka madaraka na mamlaka ni ya umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia.

Akifafanua zaidi Mnyika alisema wajibu huo unatokana na mamlaka ya Kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63 (2) na (3) na Ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya Katiba ya nchi.

Desemba 27, mwaka jana mbunge huyo aliwasilisha hoja binafsi kuhusu madai ya Katiba mpya kwa katibu wa Bunge ili ijadiliwe katika kikao cha Bunge Februari mwaka huu.

Mara baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Mnyika alisema Katiba iliyopo sasa imefanyiwa marekebisho mara 14 na kutoa mapungufu 90 ya Katiba ya sasa.

Chanzo: Tanzania Daima (10/01/2011)

No comments: