Monday, January 10, 2011

Mnyika aendelea na mchakato wa hoja

MBUNGE wa Ubungo, Bw. John Mnyika ameamua kuendelea kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu katiba kama alivyokusudia kutokana na serikali kuacha kutoa ufafanuzi wiki moja baada ya mwito wa kutakiwa kufanya
hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Bw. Mnyika alisema kutokana na Rais Jakaya Kikwete na serikali yake kuacha kutoa ufafanuzi kuhusu hoja binafsi wiki moja baada ya mwito wa kutakiwa kufanya hivyo inaonyesha bayana kwamba hakuna mpango wa kuhusisha umma.

"Inaonyesha bayana kwamba hakuna mpango wa kuhusisha umma kuanzia hatua za awali katika mchakato kupitia kuwasilisha hoja au muswada bungeni ili kuwekwa mfumo wa kisheria wa kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya," alisema.

Alisema ushahidi kuhusu serikali yake kutokuwa na dhamira ya kuandika katiba mpya inayohusisha umma na badala yake kuendeleza kuhodhi ya serikali ambayo inaweza kusababisha mapitio yenye kasoro zile zile za miaka yote, ni kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mwaka mpya mbele ya mabalozi.

Bw. Mnyika alisema kwenye hafla hiyo Rais Kikwete amerudia tena kauli ya kuunda moja kwa moja tume ya kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa maoni bila kuhusisha bunge katika hatua za msingi.

"Baada ya kauli niliyotoa ya kutaka ufafanuzi na matamko yaliyotolewa na wadau mbalimbali ya kueleza kasoro za hatua ya Rais Kikwete ya kutaka kuunda tume nilitarajia kwamba katika kauli yake ya kwanza kabisa ya mwaka huu angetumia fursa hiyo kufafanua suala husika, ikiwemo kueleza kusudio la kupeleka mapendekezo ya mchakato bungeni," alisema.

Bw. Mnyika alisema kuwa hiyo inadhihirisha kwamba Rais Kikwete anataka katiba mpya kwa maneno tu, lakini haonyeshi kwa vitendo kuwezesha mchakato husika kwa kuushirikisha umma kwa ukamilifu.

Alisema kutokana na maoni aliyopokea na utata wa kauli za serikali kuhusu mchakato wa katiba mpya, anaendelea kukamilisha taratibu za kuwasilisha hoja binafsi kwenye bunge la Februari kuhusu mchakato wa katiba mpya, na tayari alikwishawasilisha taarifa ya hoja Desemba 27 mwaka jana.

Mbunge huyo alisema kutokana na mjadala unaoendelea inaonekana bayana kwamba bado iko haja ya suala hilo la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea Ibara ya 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni ya umma.

Pia kuwa serikali inafanya kazi kwa niaba na bunge ambalo ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63 (2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Chanzo: Majira (10/01/2010)

No comments: