Friday, April 1, 2011

TAMKO LA AWALI KUHUSU MUSWADA WA MABADILIKO YA KATIBA

Nimeshtushwa na maudhui ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011 (The Constitutional Review Act 2011) uliochapwa katika gazeti la serikali toleo No. 1 Vol. 92 la tarehe 11 Machi 2011. (Muswada unapatikana hapa: http://www.policyforum-tz.org/node/7806)

Maudhui ya muswada huu yamedhihirisha tahadhari niliyotoa mara kadhaa kwamba serikali haina dhamira ya kweli ya kuhakikisha panakuwepo na mchakato mzuri wa kuwa na katiba mpya.

Muswada huo umelenga kuhalalisha yote ambayo yalitangazwa kufanywa na Rais kuhusu mchakato wa katiba mpya na kupingwa na wadau mbalimbali; sasa yanataka kupewa uhalali kwa sheria inayotaka kutungwa na bunge kupitia muswada huo.

Muswada huo unataka kumpa mamlaka Rais ya kuunda tume ya kuongoza mchakato mzima wa katiba bila kuhusisha bunge ama wadau wengine wa msingi. Muswada huo pia utaka kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa tume husika bila kushauriana na mtu yoyote isipokuwa Rais wa Zanzibar. Muswada huo unaelekeza kuwa katika kuteua wajumbe Rais atazingatia uwakilishi wa makundi ya kijamii, lakini makundi husika hayatajwi hata kwa ujumla wake na hivyo kuacha mamlaka yote ya kuamua uwakilishi kubaki kwa Rais.

Muswada huo unataka kumpa Rais mamlaka ya kutengeneza hadidu rejea za Tume jambo ambalo lilipaswa kufanywa Bunge kwa kuwa sehemu ya sheria husika ama kufanywa na mkutano mkuu wa kikatiba. Kwa kutoa mamlaka ya kuunda hadidu rejea kwa Rais mwanya umetolewa kwa mtu mmoja kuweka mipaka ya nini kinastahili kufanywa na tume wakati wa mchakato wa katiba mpya na hivyo kuminya wigo wa mabadiliko.

Muswada huo unataka Tume iwasilishe ripoti yake kwa Rais ambaye atampa nakala Rais wa Zanzibar na baadae kumwelekeza waziri mwenye dhamana kupeleka yale atayoamua Rais bungeni. Muswada huu kwa kuwa na kifungu hiki utaendeleza yaliyofanywa na marais waliopita kuhusu ripoti na mapendekezo ya tume zingine na hivyo kukwamisha mabadiliko ya kweli.

Muswada huo unataka kutoa mamlaka kwa tume itayoundwa kuitisha jukwaa (fora) ambalo litaundwa kwa ajili ya kupata maoni pekee (ad hoc) badala ya kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa Katiba (National Conference/congress) kama wadau walivyohitaji. Aidha uwakilishi katika jukwaa hilo umejwa tu kuwa ni wa kijografia na kimakundi bila kuweka bayana mnyumbuliko wa uwakilishi. Muswada huo unataka kutoa mamlaka finyu kwa jukwaa hilo kuwa ni kutoa ushauri kuhusiana na muswada; tofauti na mkutano mkuu wa kikatiba ambao ungekuwa na mamlaka zaidi katika mchakato husika.

Muswada huo unataka kutoa mamlaka kwa Rais kuitisha bunge la katiba (constituent assembly) ikiwemo kuteua wajumbe wa bunge husika. Muswada huo unataka kutoa mamlaka makubwa kwa Rais kuteua wawakilishi wa chombo kikuu zaidi katika mchakato wa katiba bila kushauriana na kundi lolote ama wananchi kuhusika katika uteuzi ama kuwa na wawakilishi walioteuliwa na makundi yenyewe mathalani vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama wa wakulima, vyama vya wanafunzi, vyama wa wafanyakazi nk. Muswada huo unataka Rais ashauriane na Rais wa Zanzibar na mwanasheria mkuu wa serikali pekee. Muswada huo unatoa mamlaka makubwa zaidi ya Rais kuamua hata kufanya bunge la kawaida kuwa ndilo bunge la katiba, jambo ambalo linaweza kurejesha udhaifu uliofanywa katika mchakato wa katiba inayotumika sasa ambapo umma uliporwa wajibu na mamlaka yake ya kushiriki moja kwa moja katika kupitisha katiba.

Muswada huo kwa ujumla haujaeleza muda wa mchakato wa katiba na vipindi vitavyotumiwa na vyombo mbalimbali katika hatua mbalimbali za mchakato wa katiba; ama kutoa mamlaka ya kuwekwa kwa muda huo kwa chombo chenye uwakilishi mpana wa umma kama mkutano wa katiba au bunge na hivyo kutoa mwanya kwa mchakato mzima kucheleweshwa.

Haya ni baadhi ya maudhui ndani ya muswada husika ambayo yamenishtusha na kunifanya nitoe tamko hili la awali wakati nikiendelea kufanya uchambuzi wa kina ambao nitautolea kauli katika hatua za baadaye.

Lengo la kutoa tamko hili la awali ni kutoa mwito kwa vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari, taasisi za dini na watanzania kwa ujumla wakiwemo wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo kufuatilia kupata nakala ya muswada huo ama maudhui yake kwa ajili ya kuujadili kwa dharura na kutoa matamko. Aidha kwa katika kauli hii ya awali naitaka serikali itoe taarifa kwa umma namna ambavyo wananchi wanaweza kupata nakala za muswada huo nyeti na sababu za serikali kupuuza maoni mengi ya wadau yaliyotolewa kabla ya kuandaliwa kwa muswada huo kuhusu mchakato unaofaa kuongoza mabadiliko ya katiba katika taifa letu.
Ikumbukwe kuwa tarehe 9 Februari 2011 nilitoa tamko kuwa nilipokea kwa tahadhari uamuzi wa Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kubadili misimamo ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kuamua kukubaliana na mwito wa kutaka mchakato husika uanzie bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika kama nilivyokuwa nikitoa mwito kwa nyakati mbalimbali.

Nilieleza kwamba nilipokea kwa tahadhari kwa kuwa bado kauli za serikali kuhusu mchakato husika zina utata kwa kuwa hotuba ya Rais Kikwete ya tarehe 5 Februari 2011 pamoja na kutaja kuwa katiba mpya itapitishwa kwa kura za maoni, haikueleza iwapo Mkutano Mkuu wa Kikatiba utaitishwa katika hatua za awali za mchakato husika. Utata huu unaongezeka zaidi kwa kuwa Waziri Mkuu Pinda akilihutubia bunge tarehe 8 Februari 2011 pamoja na kueleza kwamba muswada kuhusu mchakato husika utawasilishwa kwenye mkutano wa tatu wa bunge mwezi Aprili, ameelezea kuwa sheria husika itahusu kuundwa kwa tume.

Katika muktadha huo nilitoa kauli ya kuitaka serikali iwapo muswada unaopelekwa bungeni mwezi Aprili iwapo utaweka utaratibu wa kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba kuanzia hatua za awali pamoja na mwishowe kupigwa kwa kura kwa kura za maoni. Ni muhimu kwa tume ya mchakato wa katiba kuandaliwa hadidu rejea zake na kuundwa na mkutano wa kikatiba ambao utaweka tunu/misingi muhimu kabla ya kuanza kwa mchakato, ili tume ikusanye maoni, ipeleke rasimu kwa mkutano mwingine wa kikatiba na hatimaye katiba ithibitishwe kwa kura ya maoni. Nilitoa mwito pia kwa serikali kutoa ufafanuzi iwapo sheria husika inayokusudiwa kutungwa itagusa marekebisho ya katiba ibara ya 98 ili kutoa uhalali kwa katiba mpya kupitishwa na umma kupitia mkutano wa kikatiba na kura za maoni badala ya bunge pekee ambalo kwa sasa ndicho chombo chenye mamlaka ya mabadiliko ya katiba.

Ikumbukwe kwamba msimamo wa awali wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu mabadiliko ya katiba alioutoa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari tarehe 17 Disemba 2010 ulikuwa na kumshauri Rais aunde jopo shirikishi ili kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Kutokana na msimamo huo tarehe 19 Disemba 2010 nilifanya Mkutano na waandishi wa habari na kupinga msimamo huo na kueleza kwamba ni muhimu kwa mchakato wa katiba mpya kuanzia bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika badala ya kuundwa kwa jopo shirikishi la wataalamu kama alivyotaka Waziri Mkuu. Aidha katika mkutano huo nilipingana na azma ya Waziri Mkuu Pinda ya kutaka marekebisho ya katiba badala yake nikaitaka serikali itangaze rasmi kuanzisha mchakato wa katiba mpya. Katika Mkutano huo na waandishi wa habari nilidokeza kuwa kutokana na serikali kutoa msimamo wa kutokupeleka hoja au muswada wa serikali bungeni wa kuratibu na kusimamia mchakato husika nitalazimika kupeleka hoja binafsi bungeni ili bunge litipishe maazimio ya kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya ili hatimaye kuwezesha kutungwa kwa sheria ya kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Tarehe 27 Disemba 2010 nilitekeleza azma hiyo kwa kuwasilisha taarifa ya hoja kwa katibu wa bunge ya kutaka kuwasilisha hoja ili bunge lipitishe azimio la kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya na kupitisha utaratibu wa kisheria wa kuratibu na kusimamia mchakato mzima. Katika Mkutano wangu na waandishi wa habari siku hiyo nilieleza kwamba baadhi ya mambo ya msingi yatayozingatiwa katika hoja binafsi ni pamoja na kuhakikisha kwamba kunatungwa sheria ya kuwezesha kuitishwa kwa mkutano mkuu wa taifa wa kikatiba, tunatunga sheria ya kuwezesha tume ya kuratibu mchakato husika kuundwa kwa sheria ya bunge badala ya kuteuliwa na Rais, kutoa kwa mujibu wa sheria elimu ya uraia kwa umma kuhusu maudhui na mchakato husika na kuweka utaratibu wa kisheria wa kuwezesha kufanyika kwa kura za maoni.

Tarehe 31 Disemba 2010 Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa akatangaza kukubaliana na suala la kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya na kutangaza dhamira yake kuwa ya kuunda tume ya kusimamia mchakato husika na hatimaye vyombo vya kikatiba kufanya mabadiliko husika.
Tarehe 2 Januari 2011 nilitoa kauli yangu kwa umma ya kuitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu kauli ya Rais Kikwete na kueleza bayana iwapo serikali inakubaliana na hoja ya kupeleka suala husika ili mchakato uratibiwe na kusimamia kwa sheria itayotungwa na bunge itayaozingatia kufanyika kwa mkutano wa kitaifa wa katiba, kuundwa kwa tume kwa mujibu wa sheria badala ya uteuzi wa Rais na hatimaye kufanyika kwa kura za maoni; na nikaeleza bayana kwamba wakati nasubiria ufafanuzi wa serikali taarifa yangu ya hoja binafsi kuhusu katiba inaendelea.

Tarehe 7 Januari 2011 badala ya kutoa ufafanuzi na kueleza azma ya serikali kupeleka suala husika bungeni Rais Jakaya Kikwete akarudia tena mbele ya mabalozi kwenye hafla ya mwaka mpya kuwa anakusudia kuunda moja kwa moja tume ya kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa maoni bila kuhusisha bunge katika hatua za msingi.

Kutokana na serikali kuendeleza msimamo huo tarehe 9 Januari 2011 nilitoa tamko kwa umma la kupinga utaratibu wa Rais kuunda moja kwa moja tume ambapo ni kuendeleza hodhi ya serikali na kusababisha mapitio (review) ya katiba na hivyo kuendeleza kasoro za msingi kama zilivyojitokeza katika vipindi vilivyopita. Katika tamko langu hilo nilieleza wazi kuwa kama serikali itaendelea na msimamo wake wa kutaka kuunda tume ya Rais badala ya mchakato husika kuanzia bungeni hali hiyo itadhihirisha serikali kutokuwa na dhamira ya kuandikwa kwa katiba mpya na umma wenyewe. Kutokana na hali hiyo nilitoa tamko ya kuendelea na uamuzi wangu wa kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili mchakato husika uanzishwe kwa maazimio ya bunge na kusimamia kwa sheria itayotungwa na bunge.

Siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa bunge (ambao ulianza tarehe 8 Februari 2011 ) hatimaye serikali kupitia Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ilieleza dhamira ya kulipeleka suala la mchakato wa katiba mpya bungeni kupitia kuwasilisha muswada wa serikali na hivyo kubadili msimamo wa awali wa kutaka kuunda moja kwa moja tume ya Rais na kukubaliana na sehemu ya hoja yangu ya kutaka mchakato husika kuanzishwa na kusimamiwa kwa sheria iliyotungwa na bunge.

Wakati wote nimekuwa nikisisitiza kuwa ipo haja ya suala hili la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Rais Jakaya Kikwete akihutubia Mkutano wa CCM tarehe 5 Februari 2011 alitoa kauli kuwa Kiserikali matayarisho yanaendelea ya kupeleka Bungeni Mswada wa Sheria wa kuanzisha mchakato wa katiba mpya ikijumuisha kuundwa kwa Tume ya kuongoza mchakato huo. Aidha katika Mkutano huo Rais Kikwete aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni na katika kupiga kura ya maoni itakayoidhinisha katiba hiyo.

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisoma tamko la serikali bungeni tarehe 8 Februari 2011 alisema kwamba serikali katika kuitikia mwito wa wananchi kuundwa kwa katiba mpya imetangaza kuwa itawasilisha bungeni muswada wa kuundwa kwa tume itayoratibu mchakato wa katiba mpya katika mkutano wa tatu wa bunge la kumi Aprili mwaka 2011.
Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
30/03/2011

2 comments:

Anonymous said...

Inaelekea wameshindwa kusoma alama za nyakati. Waache wajidanganye dawa yao ipo Tahrir Square.

Barton Willilo said...

Its All about ''Change Management'' The incumbent is neither willing nor ready to change, however, change will change whoever resists time has come. Thanks John