Monday, May 7, 2012

Hatua tulizochukua kurejesha maji Golani ya Msewe; Goba bado kuna vikwazo

Jana tarehe 6 Mei 2012 tulifanya mkutano na wananchi wa mtaa wa Msewe kata ya Ubungo kuhusu mradi wa maji katika eneo la Golani taarifa ilitolewa kuhusu hatua ambazo tumechukua mpaka na kuwezesha maji kurejeshwa katika eneo la Golani, ambapo mpaka kufikia juzi tarehe 5 Mei 2012 tayari Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ilikuwa imesukuma maji kwa ajili ya wananchi wa eneo husika kuanza kupata maji.


Pia katika mkutano huo taarifa ya ukaguzi maalum wa mradi wa maji wa Golani kwa kipindi cha Novemba 2007 mpaka Machi 2012 ilitolewa kwa wananchi ambayo ilieleza kasoro zilizopo kwenye mradi ambazo zimekwamisha wananchi kupata maji kwa muda mrefu ikiwemo kutofuatwa kwa muongozo wa muundo wa kamati za maji ili wananchi waweze kuchukua hatua zaidi.

Aidha taarifa hiyo pamoja na mambo mengine ilieleza kwa kina kuhusu kuwepo kwa ‘matumizi hewa’ ya zaidi ya milioni 63, mapato ya zaidi ya milioni 89 kukusanywa kwa kutumia nyaraka zisizo sahihi na kulimbikizwa kwa deni la maji hali ambayo ilifanya Kampuni ya Maji-Safi na Maji-Taka (DAWASCO) kuwakatia maji wananchi wa eneo la Golani. Kufuatia taarifa hii maamuzi mbalimbali yalifikiwa na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2007 mpaka 2011 kwa nyakati mbalimbali eneo la Msewe-Golani limekuwa na matatizo ya maji kutokana na malalamiko ya wananchi nilifanya ufuatiliaji na kubaini kwamba chanzo cha matatizo hayo ni udhaifu katika uendeshaji wa mradi wa maji katika eneo husika.

Tarehe 26 Januari 2012 nilifanya mazungumzo ya kikazi na wawakilishi wananchi toka Kata ya Ubungo pamoja na Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na ambapo pamoja na mambo mengine ilikubaliwa hatua za haraka zichukuliwe kuwezesha wananchi wa eneo husika kupata maji.

Kufuatia mazungumzo hayo Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob, Diwani wa Viti Maalum Jimbo la Ubungo Joyce Muya na watendaji wengine wa kata na mitaa walifanya mkutano na wananchi wa eneo husika tarehe 26 Februari 2012 ambapo ilisomwa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa maji wa Golani kwa kipindi cha Oktoba 2007 mpaka Machi 2012, taarifa ambayo ilikataliwa na wananchi na kutaka ufanyike ukaguzi maalum wa mapato na matumizi ya mradi huo.

Matatizo ya maji katika Jimbo la Ubungo na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam yamedumu kwa muda miaka mingi kutokana na udhaifu wa usimamizi katika vyombo vinavyohusika na utoaji wa huduma husika. Pamoja na changamoto zilizopo katika maeneo yanayohudumiwa moja kwa moja na mabomba ya DAWASCO na DAWASA yapo pia matatizo katika miradi inayoendeshwa na vyama vya watumiaji maji pamoja na kamati za wananchi ambazo zinapaswa kusimamiwa na Manispaa.

Matatizo kama ya mradi wa Golani yamejitokeza pia katika mradi wa maji Goba kati ya mwaka 2005 mpaka 2010 hali ambayo ilihitaji kuunganisha wananchi kuweza kuchukua hatua. Kwa upande wa mradi wa maji Goba hatimaye DAWASCO ilikubali kurejesha maji kwa wananchi baada ya hatua ambazo tulichukua zilizowezesha Manispaa ya Kinondoni kuingilia kati. Mpaka sasa taratibu zinazoendelea kwenye mradi wa maji Goba ni uwekaji wa mfumo mbadala wa mabomba ya maji pamoja na mita ili kuepusha wizi wa maji na malimbikizo ya madeni kama ilivyokuwa katika siku za nyuma.

Hata hivyo, kasi ya urejeshaji wa maji imekuwa ndogo kutokana na udhaifu wa kiutendaji wa idara ya maji ya manispaa ya Kinondoni suala ambalo mamlaka husika zimetoa maagizo ya hatua za kuchukuliwa ili kuwezesha maji kurejea kwa haraka. Kwa upande mwingine, tofauti na mradi wa maji Goba hakuna kasoro za miundombinu zilizobainika mpaka sasa kwa upande wa mradi wa maji wa Golani na hivyo kufanya huduma ya maji kurejea mapema zaidi. Natoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mamlaka zote za kiserikali zinasimamiwa ipasavyo kuongeza ufanisi katika miradi ya maji.

No comments: