Sunday, July 29, 2012

Kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa kutoa maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge:

Kwa maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande mwingine, uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa serikali.

Ukiondoa tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.

Hivyo hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani. Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.

Hata baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka kama nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe 15 Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.



Nilisema bungeni kwamba “Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara”.

Mathalani, Waziri wa Nishati na Madini ameeleza bungeni tarehe 28 Julai 2012 kuwa wapo wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara zenye kulihujumu Shirika la Umeme (TANESCO) na Spika wa Bunge akahitimisha kuwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itachunguza tuhuma husika na pia kwamba inakusudiwa kutungwa kwa Kanuni za Maadili (Code of Conduct) ili kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo, Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kuwa mwaka 2008 baada ya Kashfa ya Richmond iliazimiwa katika Azimio Na. 11, kwamba “Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1995 (The Public Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa Viongozi Waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali ianze rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani na nje ya Bunge kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.”

Bunge lilitaarifiwa Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa Serikali kwamba kikundi kazi (Task Force) kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura 398) ambao ulikuwa katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge lilielezwa kuwa serikali ilitarajia kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa kumi na tisa wa Bunge la tisa. Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la tisa kama ilivyoshauriwa na kamati na mpaka kutokana na uzembe na udhaifu azimio hilo halijatekelezwa na tuhuma nyingine zimeendelea kuibuka.

Aidha, kumetolewa madai ya baadhi ya wabunge kupokea ama kudai rushwa suala ambalo nalo Spika wa Bunge ametoa uamuzi kuwa litashughulikiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Lakini Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kwamba hii si mara ya kwanza kwa tuhuma za namna hiyo kutolewa juu ya baadhi ya wabunge wa kamati mbalimbali za bunge.

Hata hivyo, kwa sababu ya kutochukua hatua kwa haraka na kwa ukamilifu tuhuma kama hizo zitaendelea kujirudia hata baada ya kuvunjwa kwa kamati ya bunge ya nishati na madini. Izingatiwe kwamba madai ya rushwa kutolewa kwa wabunge yaliwahi kujitokeza kuhusu Kamati ya Nishati na Madini na binafsi nilitoa ushuhuda kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2011, na nikatoa ushuhuda tena kwa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni mwaka 2011 kuwa yamekuwepo matukio ya kushawishi wabunge kwa rushwa hata hivyo hatua hazikuchukuliwa ama kuvunja kamati zilizotajwa au kuwachukulia hatua wahusika.

Suala hili likatajwa tena na Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila kuhusu Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na likatajwa tena na Kiongozi wa Upinzani Freeman Mbowe na Mbunge wa Kyela Dr Harrison Mwakyembe kuhusu uchaguzi wa Afrika Mashariki lakini hatua hazikuchukuliwa kuchunguza wabunge husika na kuchukua hatua. Iwapo maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 (Maarufu kama Sakata la Jairo), yangetekelezwa na wahusika wangechukuliwa hatua ingejenga nidhamu pia kwa watendaji wa wizara na mashirika ya umma kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yenye kulenga kuwaathiri wabunge kwa rushwa na maslahi mengine ya kifedha.

Katika hali inayoonyeha kwamba Serikali bado haioni uharaka na ulazima wa kuchukua hatua, wakati bunge lilipokaa kama kamati tarehe 28 Julai 2012 kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini nilitaka ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa bungeni toka yapitishwe mwezi Novemba mwaka 2011; lakini Waziri akajibu tu kwamba hawezi kufanyia kazi taarifa za magazetini, bila kujali kwamba nilichouliza hakihusu taarifa za magazetini bali maazimio ya bunge baada ya kazi iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge ambayo ilihoji wahusika na kupata pia vielelezo.

Kwa hiyo, ni muhimu Serikali na Uongozi wa Bunge ukarejea kwenye Hotuba niliyowasilisha bungeni na kuchukua hatua kwa usimamizi wa Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge juu ya masuala yote niliyoyaeleza. Pamoja na kutaja ushawishi uliokuwa ukifanywa kwa wabunge kuhusu suala la ununuzi wa mafuta ya IPTL, na ufisadi ndani ya TANESCO nilieleza pia masuala mengine makubwa kwenye nishati na madini yenye kuhusu mabilioni ya shilingi kwenye mikataba mikubwa ya umeme, madini, mafuta na gesi asili pamoja na hatua za mabadiliko ya kimfumo zinazopaswa kuchukuliwa.

Nimetoa maoni hayaleo jumapili tarehe 29 Julai 2012:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

12 comments:

Barton said...

Asante kwa maoni mazuri Mh. Endeleni kuyazungumza haya mpaka masikio ya serikali hii yazibuke maana ni kama viziwi kwa sasa

Anonymous said...

Mheshimiwa na vipi kuhusu wabunge wa CHADEMA wanao tuhumiwa kwa hizi kashfa. Kwa kuwa umemtaja Chenge hapo juu kama mtuhumiwa! Vp usitaje na hawa wa CHADEMA au ndio Uchunguzi unaendelea halafu ndio kimyaAaA.

Anonymous said...

Honestly wapenzi wa CHADEMA tumekuwa very disapointed. hatujui sasa ni nani tumuamini. Kweli CHADEMA tukiwapa nchi tutakuwa tumesolve tatizo kama dalili hizi zinajionyesha kwenu. Nashauri tu muonyeshe mko serious toeni kauli na hao wanaoshukiwa muwasimamishe muunde tume ya chama, ili kurudisha imani ya chama. Ntasikitika sana kama kweli Zitto anahusika, we have a lot of faith in him.

Msinga said...

Naamini hata kama anahusika ni ile hali ya kutegeshewa. Naomba viongozi hasa wa CHADEMA muwe macho, CCM watafanya kila linalowezekana kuchafua majina ya wale wanaona wanakubalika na jamii.

Hakuna mtu asiyetaka pesa, hata wewe unaemnyooshea kidole mwenzako kuna mazingira ukisukiwa utaingia tu labda roho wa Mungu peke yake ndio akuokoe.
Nawaombea sana na nyinyi muombe kuepuka mkono huu wa serikali usiotakia mema wananchi bali unajitaidi kutafuta kila aina ya mbinu kuendelea kuwa madarakani.
Acheni viongozi makini waongoze, ebu tuwe wazarendo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki CHEDEMA

Anonymous said...

hivi kama hali yenyewe ndo hivi kweli CHADEMA wanaweza kupewa NCHI ikiwa hata baadhi ya wabunge wao nawao wanahusika na RUSHWA na wapo mbee ktk kutetea maslahi ya wa TZ jamani kama hali yenyewe ndo hivi najitoa ktk CHAMA CHA CHADEMA bora nisiwe na chama kabisaaaaaa, inauma mnooooo, ikibidi tuwaachie tu hao hao CCM WABAKI KTK UONGOZI HUENDA labda wakajirekebisha, kwani nyie chadema mm,eshatupa wasiwasi hapo tu bado hatujawapa nchi je tukiwapa sio ndio mtakomba kila kitu ktk nchi hiii na mtaiuza kabisaaaaaaaaa

Anonymous said...

Kwa kweli wakati huu Chadema lazima wakumbuke misemo ya kiswahili kuwa "Nyati aliyejeruhiwa huwa hufa na mwindaji."
CCM iko makini inatafuta mbinu za kubaki madarakani. Kama wabunge wa CHADEMA watingia mtegoni kwa kula au kuomba rushwa au kuwa katika mazingira yenye kutia utata au mashaka kuwa nao wamekula au kuomba RUSHWA basi wanatuvunja moyo sana. MIMI nimshaamini amini 2015 RAIS atatoka CHADEMA. Na serikali hiyo ndiyo mbadala pekee. Mimi naomba TURUDI KWENYE NYAYO ZA BABA WA TAIFA kwenye maadili ya viongozi sina maana ya turudi kwenye Ujamaa ila siasa ya KUJITEGEMEA bado inafaa.Mnyika kasema yote hata kama atapuuzwa sisi tunaamini anachoshauri serikali. Bila kujali chama wala umaarufu wa mtu wote waliohusika wajiuzulu kisha wawajibishwe mahakamani.
DUCE

Msigwa Elias said...

Jamani 2cchangie kwa kuwahukumu watu ambao bado hatuna uhakika km wamehucka au la. Kumtaja Chenge ktk hili haina maana kwamba kamhucsha bali alikuwa akitolea mfano wa kuteua viongozi wa kucmamia rasilimali za umma ilhali wana kesi mahakamani. Naomba kitu ki1, sote ni binadamu, km kweli kuna viongozi wa CDM wamehucka bac km chama kiwachukulie hatua madhubuti ili kulinda heshima ya chama.

Qamara Antto Qamara said...

Serikali ya CCM wakati wa mwisho kutawala ni huu. Dalili zote zinaonyesha mwisho wa CCM ni Huu.Kutawala miaka 50 si tija tija ni kuondoa matatizo na wanachi wapte ubora na unafuu wa maisha.
-Idadi ya wajinga wasiojua kusoma inaongezeka
-Idadi ya wasio na kazi inaongezeka.-Idadi ya vifo inaongezeka .- Idadi ya fukara inaongezeka.- Uporaji wa ardhi ya umma unaongezeka .- wageni wanapata heshima kuliko wazawa.-Kila dalili inaonyesha haja ya kuikomboa Tanzania mara ya pili haja hiyo iko wazi.Ukombozi utaletwa na CHAMA MAKINI CHADEMA.
Japo wachache bungeni matunda tumeyaona.
RUSHWA:
Katika hili natoa angalizo wabunge na wanachama wa chadema wanaonong'onwa kuhusika Chonde chonde wajibikeni Ndugu zangu msisubiri kuaibishwa kwa kutajwa. tunajua huuni Mtego wa CCM ili mfanane nao umewanasa. Laumuni nafsi zenu na tamaa zenu.
Chama CHADEMA kiwawajibishe hao ili tusifanane na CCM. HARAKA waondoeni hao wabaki wanachama wa kawaida.
Msiogope kugombea viti hivyo tena.

Anonymous said...

msinga,kutegeshewa ndiyo kitu gani? kama kuna mtu anahusika anafaa kushughulikiwa kama waalifu wengine tu!achani unafiki.wala rushwa ni ccm tu wakiwa CDM wametegeshewa!ni upuuzi kutetea rushwa

Anonymous said...

Hapa bunge lilipotufikisha ni patamu kweli. Unajua kuna hii kasumba ya watanzania kuishi kwa kuamini kuwa ukiwa na nafasi ya juu unaweza kujifanyia chochote na usiguswe. Pia tabia ya watu kugombea nafasi wakiwa na lengo la kutajirika kwa milungula ndio hasa inajidhihirisha.
Kwa Chadema, ni wakati wa kuchukua hatua kwa yeyote anayetajwa kuhusika; hii itakuwa chachu kwa wapenda mabadiliko ya kweli Tanzania itajenga heshima.

Ipyana Mwakamela said...

Nadhani kama nimemuelewa vyema Mheshimiwa Mnyika katika maoni yake hajasimama upande wowote wa kutetea uovu huu wa RUSHWA bila kujali aliyehusika katoka ndani ya Chadema, Cuf, UDP, TLP ama CCM. Kamtaja Chenge kama mfano tu wa jinsi gani hakuna userious katika kuchukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa na hivyo alikuwa anaweka mkazo tu kwamba hali kama ile isiendelee kujitokeza kwani safari hii anashauri MAAMUZI makubwa yachukuliwe bila kigugumizi.

Ningependa tu kuwashauri WATANZANIA wenzangu kwamba tunapochngia mambo kama haya tujitahidi kuweka itikadi zetu pembeni maana ukweli ni kwamba RUSHWA inabaki kuwa adui wa haki bila kujali imetendwa na nani. Hivyo basi kila anayetenda anapaswa kuchukuliwa hatua za MFANO ili wengine watambue lakini kwa kuachiwa na kuendelea na majukumu mengine nyeti ni kuonyesha dhahiri kwamba suala la RUSHWA halichukuliwi kama ni donda baya.

Hatuna budi kuungana katika hili kuhakikisha wale wote waliohusika wanachukuliwa HATUA kali za kisheria bila kupindisha ili liwe fundisho kwa viongozi wengine wenye mfano huo. Suala la RUSHWA lisibebe itikadi kamwe tunapolijadili kwani linaumiza watu wa itikadi zote hata wasio na vyama na watoto wadogo wasiojua lolote.

Kuhusu kutawala nchi sidhani kama lina mantiki yoyote kwamba tunataka kubadilisha utawala kwa sababu tumedhani vyama vingine vimejaa MALAIKA. Hata TANU ilipochukua nchi kutoka kwa watawala wa Kiingereza hakuna mtu alitegemea kwamba kutakuwa na UFISADI w kunuka kama hivi leo hii. Lakini ikumbukwe tu kwamba CCM kama chama hakina matatizo bali wale waliomo ndani ya chama kwa kukidhi haja za miili na nafsi zao wamekinajisi Chama. Ndio maana hata ukisoma IMANI za mwanaTANU zilikuwa ziko bayana, Sera za CCM hazina kasoro kwa jinsi zilivyoandikwa bali tatizo kubwa ni uzembe katika utekelezaji wake, na hiki ndicho kinaigharimu CCM.

Baba wa Taifa hili Mwalimu Nyerere pia aliwahi kukiri kwamba "msijidanganye kwamba wakati wa utawala wangu hakukuwa na rushwa" mwenyewe anadai Rushwa ilikuwepo hata wakati wake lakini kilichoipunguza kasi ni UKALI ambao ulikuwepo katika sheria za waliokutwa na makosa ya Rushwa. Hawakubariki RUSHWA enzi zao lakini kwa sasa ni kama tumebariki maana hata watu wakituhumiwa hawachukuliwi tena sheria zaidi ya kujiuzulu nafasi zao kwa muda na kisha baadaye wanarejeshewa madaraka taratibu taratibu.

Katika hili tusiangalie ni nani kahusika na katokea chama gani bali tuwatazame wote kama wahalifu wanaofanana kwa makosa na wafanane kwa adhabu pia. Hakuna suala la kutegeshewa walakuamua kwa mawazo yako. Kosa linabakia pale pale na adhabu kali itolewe ikiwezekana tuwaone waheshimiwa hawa watakaobainika wamevaa zile sare za Magereza na wakifanyishwa kazi kama wengine, katu wasiwekewe madaraja kwa nyadhifa zao kwani hawastahili heshima tena. China na Japan wao hawana madaraja ya watuhumiwa wa Rushwa wote wanapewa adhabu inayofanana na ndio maana nidhamu ipo.

Huu uwe ni wakati muafaka wa Serikali kuhakikisha inakunjua makucha yake na pasiwepo na masuala ya kulindana tena maana hawa watakaobainika watakuwa wamekosa adabu kwa mhimili kama BUNGE hawastahili heshima tena. Nakumbushia tu kwamba uchekeweshaji wowote wa hukumu katika kesi zao utalipeleka taifa pahala pabaya zaidi. Haya tunayoyaona leo ni uzembe na udhaifu wa sheria zetu kuuma ipasavyo.

RUSHWA isiwe na chama, Dini wala Kabila. TUICHUKIE RUSHWA, TUWACHUKIE WALA RUSHWA. Inanyima haki watu wengi sana na INAUA.

Anonymous said...

Kama "Mh. Kikwete" angekuwa msafi asingekubali kuendelea kukaa na uchafu katika "SIRIKALI" yake,lakini kwasababu nae ni miongoni mwao anaogopa ataumbuka!