Monday, February 25, 2013

Mnyika amuweka Maghembe kitanzini

NA RICHARD MAKORE

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amemuweka katika wakati mgumu Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, baada ya kutoa hadharani namba ya simu ya waziri huyo ili wananchi wamuulize ni lini atatekeleza ahadi ya kuwapatia huduma ya maji wananchi wa jimbo hilo.

Mnyika alitoa namba ya simu ya Profesa Maghembe na Naibu wake, Dk. Binillith Mahenge, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Goba mwisho na kuwataka wananchi kuwauliza viongozi hao wakuu wa Wizara ya Maji ni lini watapatiwa huduma ya maji ambayo imekosekana kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Mnyika alisema Profesa Maghembe akihututubia wananchi hao aliwapa namba ya simu ‘feki’ na kwamba alifanya hivyo kutokana na kuwadharau.

Februari 17 mwaka huu, Profesa Maghembe akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Goba mwisho alikaririwa akisema kwamba huduma ya maji ingeanza kupatikana Februari 20, mwaka huu, lakini hadi kufikia juzi ahadi hiyo haijatekelezwa.

Profesa Maghembe alikaririwa akisema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo ina funguo za kufungua maji ama kuyafunga na kuwataka wananchi wa Kata ya Goba kumuamini kwamba Februari 20, mwaka huu wangepata maji.

Mnyika alisema ni aibu kwa Waziri akiwa na viongozi wa kitaifa wa CCM kutoa ahadi hewa na kwamba ataongoza maandamano makubwa ya wananchi wa jimbo lake kuvamia ofisi za Profesa Maghembe kwenda kudai maji.

Aliwaambia wananchi wa Goba kukubali kuungana na wenzao wa maeneo mengine katika jimbo hilo Machi 16, mwaka huu kwenda wizarani kwa Profesa Maghembe kudai huduma ya maji.
Alisema wananchi wa Jimbo la Ubungo wana haki ya kupatiwa huduma ya maji na kuitaka serikali iache mchezo wa kuwadharau kwa kuwapa ahadi hewa na za uongo.

“Profesa mzima kama Maghembe hawezi kuja mbele za wananchi wenye akili zao timamu na kusema Jumatano ijayo maji yatatoka yaani (Februari 20) huku akijua ni ahadi hewa, hii ni aibu kubwa kwa serikali ya CCM,” alisema Mnyika, ambaye katika Mkutano wa 10 wa Bunge aliwasilisha hoja binafsi akitaka serikali iboreshe huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam, lakini hoja hiyo iliondolewa baada Profesa Maghembe kuifanyia mabadiliko ili isijadiliwe na Bunge.

Alisema tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji linatokana na serikali kushindwa kuwa wabunifu na badala yake wameshindwa kuboresha miundombinu iliyokuwapo tangu nchi ipate uhuru mpaka sasa.

Kwa mujibu wa Mnyika, ili eneo la Goba lipate huduma ya maji, ni lazima serikali ikubali kutumia kodi za wananchi kubadilisha mabomba yaliyowekwa zamani na kuweka mapya yenye ukubwa.

Tangu alipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010, Mnyika amekuwa akitumia muda wake mwingi kushughulikia kero ya maji katika jimbo hilo.

Mara kadhaa amekuwa akiwaongoza wapiga kura wake kuwashinikiza viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa wanapatiwa maji.

Mwaka jana Mnyika aliwaongoza wapigakura wake takribani 200 kwenda makao makuu ya ofisi za Kampuni ya Majisafi na Majitaka (Dawasco) kudai maji.

Kutokana na mamlaka husika kushindwa kushughulikia tatizo hilo, mwaka jana Mnyika aliwasilisha malalamiko kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora akilalamikia wananchi wake kunyimwa haki ya kupata maji.

Hatua ya Mnyika kutoa namba za simu za Waziri Maghembe na Naibu wake ni mfululizo wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoa namba za viongozi wandamizi wa serikali kwa wananchi ili wawashinikize. 

Baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 10 wa Bunge, viongozi wa chama hicho walifanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Temeke Mwisho, jijini Dar es Salaam na kutoa hadharani namba za Spika wa Bunge, Anne Makinda, na Naibu wake, Job Ndugai.

Viongozi hao waliwataka wananchi kuwapigia simu Makinda na Ndugai kuwashinikiza wajiuzulu kwa madai ya kushindwa kuliendesha Bunge kutokana na kukipendelea CCM na kuukandamizi upinzani.

Makinda na Ndugai baada ya namba zao za simu kuwekwa hadharani walipata wakati mgumu kutoka kwa wananchi ambao waliwatumia ujumbe mfupi wa simu (sms) na nyingine ukidaiwa kuwa ulikuwa wa matusi.

Inadaiwa kuwa Makinda alipokea simu na sms takribani 600 huku Ndugai naye akithibitisha kupigiwa simu nyingi na sms za kumtukana.


Chanzo gazeti la NIPASHE 25/02/2013: http://www.ippmedia.com/frontend/index.php?l=51618 

No comments: