Monday, July 29, 2013

Hali tete na tata ya kituo cha mabasi cha Ubungo (UBT)- Hatua ambazo nimeanza kuzichukua

Katika siku za karibuni nimepokea malalamiko kuhusu hali tete na tata katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) kinachosimamiwa na kuendeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam. 

Kufuatia malalamiko hayo, nimechukua hatua zifuatazo mpaka sasa: Mosi, tarehe 15 Julai 2013 nilifanya ziara ya ghafla kujionea hali halisi, sehemu ya ziara hiyo inaweza kutazamwa kupitia: 
http://www.youtube.com/watch?v=JuPGoz-JI-I , ambapo nilibaini kwamba hatua za haraka zinahitajika. 

Nimeshuhudia hali ya uchafu ikiwemo utiririkaji wa maji machafu ndani ya Kituo cha Mabasi ambayo yanatuama na hadi kubadilika rangi na kuwa ya kijani ambapo ni hatarishi kwa abiria na watu wanaofanya shughuli zao ndani ya kituo. Pia, kuna vyoo vichache ukilinganisha na idadi ya abiria na watumiaji wengine wa Kituo. Hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Nimejulishwa hali ya usalama ndani ya kituo ni tete; usalama ndani ya kituo ni mdogo sana kwa abiria na nimepewa taarifa za matukio ya uhalifu ambayo yamesababisha pia madhara kwa abiria.

Nimetembelea kituo na kukuta kuna usumbufu mkubwa sana kwa abiria na watumiaji wengine wa Kituo baada ya maeneo ya awali ya kupumzikia kwa abiria na wasindikizaji kubomolewa. 

Nimepokea malalamiko kwa abiria wanaosubiri usafiri kwa muda mrefu na wafanyabiashara wengine wanaofanya shughuli zao ndani ya Kituo na hakuna utaratibu wa upatikanaji wa chakula kama awali. 

Nimeelezwa malalamiko ya mawakala wa mabasi juu ya utaratibu uliowekwa ya kwamba ulipitishwa kwa kuhusisha wamiliki wachache wa makampuni ya mabasi na hivyo kuibua usumbufu kwa makampuni pengine pamoja na kupunguza ajira za waliokuwa wakifanya kazi na makampuni hayo.

Nimebaini kwamba pamoja na hali hiyo tete na tata ya Kituo wananchi wanaendelea kutozwa kiingilio kile kile katika kituo pamoja na kutopata huduma zinazostahili.

Orodha ya masuala yanayodhirisha hali tete na tata katika kituo ni ndefu hivyo nitawasilisha maelezo na vielelezo zaidi kwenye kikao hicho maalum/dharura kitakachoitishwa.

Pili, kufuatia ziara hiyo ikiwa sehemu ya kazi ya kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali tarehe 24 Julai 2013 niliwasilisha barua kwa Mkurugenzi wa Jijikuitishwe kikao maalumu/dharura cha Kamati ya Fedha na Uongozi na hatimaye Baraza la Madiwani kuwezesha maamuzi kufanyika na hatua za haraka kuchukuliwa juu ya hali tete na tata katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT).

Kupitia barua hiyo nimemweleza Mkurugenzi wa Jiji kwamba hatua za haraka zisipochukuliwa kuhusu hali hiyo tete na tata inaweza kusababisha maafa/majanga au kuibua kwa mgogoro/malalamiko baina ya Serikali na Wananchi. 

Aidha, nimependekeza Halmashauri ya Jiji irejee pia Hoja binafsi niliyoiwasilisha mwaka 2011 na kuwasilisha taarifa ya masuala ambayo hayajatekelezwa mpaka hivi sasa ili yajadiliwe na kushughulikiwa.

Itakumbukwa kwamba kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 Mkurugenzi na Meya wa Jiji walinukuliwa wakisema kwamba Kituo hicho kingehamishiwa katika eneo la Mbezi Luis kuanzia Januari 2013 kupitisha ujenzi unaoendelea wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) hata hivyo zaidi ya miezi sita imepita bila ahadi hizo kutekelezwa.

Kwa upande mwingine, matatizo yanayoendelea sasa yangeweza kuzuilika iwapo mapendekezo yote ya hoja binafsi yaliyowasilishwa na Mbunge mwezi Mei 2011 kuhusu kituo cha Ubungo yangetekelezwa kwa wakati na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam. 

Katika ya maazimio ambayo nilipendekeza yapitishwe wakati huo ni kufanyika tathmini tangu mwaka huo wa 2011 kuhusu eneo ambalo lilitarajiwa kuchukuliwa na Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (DART) hatua ambayo ingewezesha maandalizi ya kituo mbadala cha kudumu kufanyika kwa wakati.

Kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali; katika muktadha huo, iwapo una maoni/mapendekezo ya hatua za ziada zinazopaswa kuchukuliwa, tafadhali tupatie kupitia mbungeubungo@gmail.com au wapatie wabunge wengine wa Mkoa wa Dar Es Salaam au madiwani wa Jiji letu. Maslahi ya Umma Kwanza.

John Mnyika (Mb)
27/07/2013

1 comment:

Anonymous said...

Habari Mhe. Samahani kwanza kwa kuwa nje ya Comment ya mada husika, mimi ni mwananchi wako wa jibo la Ubungo, niko maeneo ya king'ongo, naomba nitoe lalamiko kuhusu visima vilivyochimbwa na DAWASA ambavyo tulitegemea vingekuwa mkombozi wetu katika tatizo la maji, lakini matokeo yake tangu Mkuu wa Mkoa avizindue vizima hivyo havisaidii wananchi bali vimezidisha kero ya maji kwani hiyo kamati ambayo imeteuliwa na Mwenyekiti wa kijiji, imevifanya visima hivyo ni mali yao, na mpaka naandika malalamiko haya Mhe. wananchi wanataabika hawapati maji na hawaelewi hatima yao. Tunaomba utusaidie Mhe. kwani wakina mama wanataabika sana ndoo ya maji ya bomba ni shilingi 400/=, wakina mama wanaamua kwenda mto Mbezi kutafuta maji ambayo si salama.