Thursday, September 12, 2013

Mnyika ahoji ziliko fedha za DECI

na Shehe Semtawa

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu, kuwaeleza waliokuwa wanachama wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) fedha zao zilizotaifishwa na serikali kutoka kwenye taasisi hiyo ziko kwenye akaunti gani.

Mnyika alisema kuwa wakati sakata la DECI linaanza mwaka 2009, serikali ilitaifisha jumla ya sh bilioni 19, sawa na asilimia 40 ya fedha zote ambazo wanachama wa taasisi hiyo iliyokuwa ikiendesha na kusimamia mchezo wa upatu walikuwa wakidai.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara juzi Mtaa wa Mavurunza, Kata ya Kimara baada ya kuulizwa swali na mmoja wa wananchi aliyetaka kujua hatima ya fedha zao, Mnyika alitoa tahadhari kuwa danadana inayotaka kufanywa na serikali inaweza kutia shaka kuwa fedha hizo hazipo.

”Sasa naomba nimjibu yule mwananchi aliyetaka kujua hatima ya fedha za DECI. Mtakumbuka hili suala nimekuwa nikitaka majibu yake bungeni, lakini kila mara wanatumia kisingizio kuwa suala hili liko mahakamani.

“Juzi baada ya hukumu kutoka tumemsikia Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu akisema hawawezi kuwalipa wananchi walioweka fedha zao DECI,” alisema.

Kama wanasema waliocheza DECI nao ni watuhumiwa, walipaswa kuhukumiwa, Gavana hasemi hizo fedha sh bilioni 19 ambazo serikali ilizitaifisha na kuwekwa BoT ziko kwenye akaunti gani.

“Kwa sasa mahakama imesema mlipwe, serikali ndio walizitaifisha na kuziweka kwenye akaunti BoT, wanapata wapi kigugumizi cha kuzilipa hizo asilimia 40 ambazo tayari zipo?” alihoji.

Mbunge huyo alisema kuwa wananchi waliopanda fedha zao wana haki ya kulipwa kwa sababu zipo, zimeshikiliwa kwenye akaunti na serikali.

Alisema kuwa fedha hizo zinapaswa kurejeshwa kwa msingi kwamba pamoja na mahakama kuwahukumu waendeshaji wa DECI kuwa wahalifu, haikuwahukumu washiriki.

Aliongeza kuwa DECI ilisajiliwa na serikali kupitia viongozi wake akiwamo Waziri wa Fedha na Uchumi wa wakati huo, Mustafa Mkulo na kuhamasisha watu kujiunga.

Katika mwendelezo wa ziara yake jana, Mnyika alimtaka Diwani wa Kata ya Msigani, Logart Mbowe (CCM) kufuatilia haraka nyaraka zinazoonesha gharama za manunuzi ya vifaa vya ujenzi (BOQ) wa daraja lililoko Mtaa wa Msigani, wilayani Kinondoni.

Mnyika alitoa kauli hiyo baada ya kuelezwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Rems Lutumo (CCM) kuwa ujenzi wa daraja hilo anautilia shaka kwa kuwa hadi unafikia hatua hiyo hajui gharama zake.

“Ifuatilieni hiyo BOQ haraka, pia ni lazima kuwekwe kibao kinachoonesha kuwa daraja hilo lina uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa tani ngapi,” alisisitiza Mnyika.

Awali, Lutumo alisema hadi sasa ofisi ya mtaa huo haijui gharama halisi za ujenzi huo, huku wananchi wakihitaji kujua kwa sababu ni haki yao.

Mkazi wa mtaa huo, Said Msati, alisema daraja hilo limejengwa chini ya kiwango, bali viongozi hao walishindwa kumueleza mbunge ukweli, hatua aliyodai inatokana na tofauti zilizipo kati ya diwani na mwenyekiti wa mtaa huo.

Alisema miradi mingi ya maendeleo inakwama kukamilika kutokana na tofauti zao hizo, huku akitolea mfano wa ujenzi wa kisima, aliodai unakwenda taratibu huku diwani akidaiwa kukalia fedha.

Kuhusu kero ya maji, Katibu wa kamati ya maji ya Msigani na Malambamawili, Evetha Nchunga, alitoa taarifa kuwa wakazi wapatao 65,000 wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la maji tangu kujengwa mabomba ya Mchina miaka minne sasa.

Alisema hivi sasa wakazi hao wamekuwa wakitumia maji ya mifereji ambayo si salama kwa afya zao hususan watoto ambao hawana tahadhari.

Chanzo: TanzaniaDaima http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=53790

1 comment:

emma said...

Nikikumbuka DECI nakosa amani kabisa. Ujasiriamali kweli unachangamoto.