Friday, January 31, 2014

Mwito kwa wananchi kutoa maoni kuhusu sheria ndogo

 
Nimerejea jimboni kikazi, pamoja na ufuatiliaji kuhusu kasoro za ujenzi unaendelea katika Barabara ya Morogoro na matengenezo yanayohitajika katika barabara zinaunganika na barabara hiyo katika maeneo ya pembezoni kupunguza foleni, lipo suala linalohitaji mjadala na maoni ya haraka toka kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Tangu mwaka 2013 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa katika mchakato wa kutunga sheria ndogo nne: ya matumizi ya barabara, ushuru wa masoko, ada na ushuru na ushuru wa huduma. Mwanzoni mwa mwaka huu 2014 katika kikao cha Baraza la madiwani ilibainika kwamba sheria hizo zilikaribia kupitishwa bila ya ushirikishwaji wa kutosha wa wadau na wananchi.

Halmashauri iliongeza muda wa kupokea maoni; hata hivyo muda ukiwa unaelekea ukiongoni, ikiwa imesalia takribani wiki moja, tathmini ya ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo inaonyesha kwamba sheria hizo hazijasambazwa vya kutosha kwa wananchi na wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao katika kata na mitaa mbalimbali.

Hivyo, ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo leo tarehe 31 Januari 2014 itafanya kazi ya kusambaza Sheria hiyo kwa njia mbalimbali kwa ajili ya wadau na wananchi kupitia na kutoa maoni yao. Mkazi wa Jimbo la Ubungo anayehitaji kutoa nakala anaweza kuwasiliana na Katibu Msaidizi Aziz Himbuka kupitia 0784379542 au 0715379542 au kwa kuwasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni moja kwa moja.

Sheria ndogo ya matumizi ya Barabara pamoja na mambo mengine inapendekeza utaratibu kuhusu maegesho, usajili wa teksi, usajili wa vituo vya teksi, usajili wa mikokoteni, uoshaji wa magari, ufungaji wa barabara kwa ajili ya sherehe, misiba na shughuli zingine na kuweka utaratibu wa makosa na adhabu.

Kwa upande wa mikokoteni, sheria inapendekeza ada ya usajili kuwa elfu ishirini kwa mwaka. Kwa upande wa kuosha magari sheria inapendekeza kwamba atayekutwa anaosha gari eneo ambalo halijatengwa maalum kwa kazi hiyo atatozwa faini ya elfu 50, asipokuwa nayo gari itavutwa na kuhifadhiwa na ikipita siku 30 bila kuchukuliwa gari husika litapigwa mnada.

Sheria ndogo ya ushuru wa masoko inaweka utaratibu wa usimamizi wa masoko, usajili wa biashara, udhibiti wa nidhamu sokoni, usafi wa masoko, uingizaji wa bidhaa sokoni, ukusanyaji wa kodi, ada na ushuru na adhabu ya faini ya elfu hamsini au kifungo cha miezi sita kwa makosa katika maeneo ya masoko.

Sheria ndogo ya ada na ushuru inafanya mabadiliko kwa kuongeza viwango vya ada za kubadili matumizi ya ardhi, kugawa viwanja, mashamba na kurekebisha michoro. Pia, inafanya marekebisho kuhusu viwango vya ushuru wa kupima na kukagua nyama machinjioni, ada za ramani ya majengo na kuhusu vituo cha mafuta na maegesho.

Sheria ndogo ya ushuru wa huduma inakusudiwa kusitisha matumizi ya sheria ndogo ya Dar Es Salaam City Commission (City Service Levy) by Law 1997 katika Manispaa ya Kinondoni kufanya mabadiliko kuhusu utaratibu wa ukusanyaji ushuru (uwasilishaji wa taarifa, uwezo wa kuingia kukagua jengo, uwekaji kumbukumbu za biashara, uteuzi wa mkusanyaji) na kueleza makosa na adhabu mpya.

Aidha, leo tarehe 31 Januari 2014 tutambelea sampuli ya mitaa katika kata mbalimbali kwa ajili ya kukutana ana kwa ana na wadau wanaoguswa na sheria hizo katika masoko, vituo vya daladala/bajaj/bodaboda/taxi, maeneo ya biashara na baadhi ya makazi ya wananchi kwa ajili ya kusambaza nakala waweze kuzipitia na kuwasilisha maoni kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Aidha, kwa nyakati mbalimbali nimependekeza kutungwa kwa sheria nyingine ndogo mpya au kuzifanyia marekebisho zilizopo katika maeneo mengine saba yenye kugusa wananchi hata hivyo kasi ya utekelezaji imekuwa ikisuasua. 

Masuala hayo ni pamoja na sheria ndogo kuhusu maeneo ya umma ya wazi (public spaces), uanzishaji na usimamizi wa miradi ya maji ya jumuiya, mifuko ya maendeleo ya wanawake na vijana, kuwezesha upimaji wa haraka wa viwanja na upangaji wa makazi, kuboresha mfumo wa ulinzi shirikishi na polisi jamii, kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi za majengo na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika Serikali za Mitaa.

Mjadala kuhusu sheria ndogo nne zilizopendekezwa uwezeshe kutungwa kwa sheria zingine saba katika maeneo niliyoyaanisha na mengine yatayopendekezwa na wananchi ili Halmashauri iwe na nyenzo za kusimamia maendeleo endelevu.


Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)

31/01/2014
Jimboni Ubungo
 

No comments: